Pages

Friday, 7 March 2014

BODI YA LIGI YATOA ADHABU YA FAINI KWA :


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni 1/- klabu ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria kuwa timu hiyo inaendekeza ushirikina uwanjani.

Klabu ya Simba inasemekana kufanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000/- na faini nyingine ya sh. 500,000/- wamepigwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kwa kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.

Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000/- kwa kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa kidole.

Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 300,000/- kwa kitendo cha washabiki wake kuingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Nazo klabu za Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya sh. 500,000/- kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.

Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000/- kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000/- kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.

Pia mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000/- kwa kosa la kupigana uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000/- kwa washabiki wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.

Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000/- kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment