HOMA ya pambano la watani wa jadi katika muziki wa dansi nchini kati ya Mlimani
Park 'Wana Sikinde' na Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' litakalofanyika siku ya
Krismasi imeanza kupanda kwa bendi hizo kujificha kambini na huku wakipigana
vijembe.
Bendi hizo kongwe nchini zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika onyesho
litakalofanyika kwenye viwanja wa TCC Club Chang'ombe, Temeke Dar es Salaam
katika kunogesha sikukuu hiyo ya Krismasi.
Katika kuonyesha wamelipania pambano hilo bendi ya Sikinde tayari imeiendea
Msondo wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kuweka kambi yao na wamewatahadharisha
'mahasimu' wao hao wasije wakatoa visingizio baada ya kugaragazwa kwenye
onyesho hilo.
"Sisi tumeamua kuweka kambi yetu mjini Bagamoyo ambako tutatua viwanja vya
TCC kutokea huko ili kuisambaratisha Msondo, na tunataka wajipange sawasawa ili
wasije wakatoa visingizio tena kwa maana kama vyombo vipya bendi zote imepewa
na Konyagi," Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo alisema.
Milambo alisema mashabiki wa dansi wajitokeze kwa wingi kushuhudia namna gani
wanavyowachachafya wapinzani wao hao, ikizingatiwa hawajakutana kwa muda tangu
mwaka jana.
Upande wa Msondo kupitia Meneja wao, Said Kibiriti, alisema hawana haja ya
kutaja mahali kambi yao ilipo isipokuwa wamejiandaa kuwatoa nishai wapinzani
wao siku ya onyesho hilo litakaloanza saa nane mchana.
"Sisi hatuna mchecheto wowote na mpambano huo, tunaendelea kujifua kimya
kimya mahali ambapo siwezi kupataja kwa sasa," alisema Kibiriti.
Naye muimbaji anayekuja juu wa bendi hiyo ya Msondo alitokea Sikinde, Athuman
Kambi, alisema amejipanga kuonyesha umahiri wake katika mpambano huo baada ya
kufanya hivyo wakati akiwa Sikinde dhidi ya Msondo kwenye ukumbi wa Diamond na
kuwawehusha mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
"Najua watu watataka kuona nafanya kitu gani dhidi ya bendi yangu ya
zamani iliyonitangaza vyema, wasiwe na hofu waje Desemba 25 waone nini nitakachofanya
TCC Club Chang'ombe," alisema Kambi.
Mpambano huo wa Sikinde na Msondo umeandaliwa na kampuni ya Bob Entertainment
na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi, gazeti la NIPASHE, Integrated
Communications, CXC Africa na Salute5.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment