Bila ya
kuwataja kwa majina, Zitto alisema watu hao ni wale walioshika nyadhifa za
uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri
wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya
Nishati na Madini.
Wengine ni
mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa
Serikali, makamishna wa nishati na walioshika wadhifa wa Ukurugenzi wa Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC.
Baada ya
kutolewa kwa hoja hiyo, Serikali iliunda kikosi kazi cha kufuatiliwa fedha
hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema akiwa ndiyo kiongozi
wa timu hiyo.
Katika mahojiano ambayo Jaji Werema alifanya na Mwananchi mapema
Januari mwaka huu, alisema hadi kufikia Aprili mwaka huu, wangekuwa na jambo la
kueleza umma kutokana na uchunguzi huo.
Werema abainisha kuwa Serikali
iliandika barua kwa vyombo vya Uswisi vinavyohusika na masuala ya fedha,
wakivitaka viwape taarifa za akaunti za Watanzania.
“Walitueleza
tunachojaribu kufanya ni sawa na mtu anayevua samaki, anajua kabisa kuwa
baharini kuna samaki, lakini mahali walipo hapajui. Walitaka tuwape majina ya
wahusika tunaowataka, kisha kuwaeleza kwa nini tunazitaka fedha hizo,” anaeleza
na kuongeza:
Anasema
katika kufuatilia hilo, wangekwenda mbali zaidi kwa kufuatilia majina yote
watakayopata na kuangalia wahusika kama wana kibali cha Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), kuweka fedha hizo katika nchi hiyo.
Anasema kuwa
Zitto Kabwe ambaye ndiye aliyeeleza suala hilo bungeni ni mtu muhimu kwao,
hivyo angeshirikishwa ipasavyo.
“Tukipata
taarifa kwa sasa tunaweza kwenda kwenye hizo benki, hatutaki kwenda tu na
kusema tupewe majina ya Watanzania walioweka fedha zao huko, ukifanya hivyo
kama huyo mtu atakuhurumia sana sana atakufukuza, lakini kama ni mweledi
atakuitia polisi,” anasema Werema.
Kauli hiyo
ya Werema, ilikuja siku chache baada ya Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave
kusema Serikali ya Tanzania haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na
kupata ukweli wa mabilioni ya fedha yaliyofichwa nchini humo.
Chave anasema: “Uswisi iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua
uhalali wa fedha hizo na endapo zikigundulika ni fedha chafu basi tutazirejesha
nchini.
Serikali ya
Uswisi haina tatizo kwani tumeshafanya hivyo kwa nchi za Ufilipino na Nigeria,
hivyo tutafurahi na Tanzania kama tutamaliza suala hili,” alisema balozi huyo.
Mbali na balozi huyo, Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf mwisho wa
Oktoba alifanya mazungumzo na gazeti hili ambapo pia alizungumzia suala hilo.
Alipoulizwa
kama anafahamu kuwa, kuna hoja binafsi ndani ya Bunge la Tanzania juu ya fedha
zilizofichwa nchini mwake, alisema kuwa hilo siyo suala la Bunge, bali ni suala
kati ya Serikali ya Uswisi na ile ya Tanzania.
“Serikali yetu ni ya uwajibikaji. Nina uhakika kama Serikali itakuwa
imeelezwa itafanya kazi yake,” anasema.
Kauli ya Werema aliyoitoa Januari
iliwapa Watanzania matumaini, lakini mpaka Bunge la Aprili linapita hakuna kilichofanywa.
Baada ya hapo, Zitto alinukuliwa
mara kadhaa akiahidi kuwa siku moja atayataja majina ya watu walioficha fedha
hizo, huku akiilaumu Serikali kutokufanya kazi yake kama ilivyotarajiwa katika
kufuatia fedha hizo.
Zitto asisitiza
Juma lililopita
akizungumza bungeni, Zitto anaihoji Serikali akiktaka ieleza sababu za
kuchelewesha ripoti ya ufichaji wa fedha nje ya nchi.
Anasema tatizo ni utayari wa Serikali katika kulishughulikia jambo
hilo na kuhakikisha linaisha.
Anasema kuna
mikataba kwa ajili ya kupeana taarifa na Afrika zimesaini ambazo ni Ghana,
Afrika Kusini na Nigeria, lakini Tanzania haijaisaini.
“Utapataje taarifa wakati hujasaini mkataba kama huu, mjadala sasa ni
mabilioni ya fedha za Uswisi lakini ni zaidi ya mabilioni ya Uswisi. Uswisi
kuna Sh319 bilioni, Genes, kisiwa kimoja nchini Uingereza kina zaidi ya
trilioni moja za Watanzania na ukikaa mtajadili na Watanzania na wanapenda vitu
vyepesi vyepesi.”
Majibu ya Werema
Jaji Werema
akijibu hoja za Zitto mbali na kuomba kuongezewa miezi sita ili wamalize suala
hilo, anapinga suala la Tanzania kusaini sheria ya kubadilishana taarifa za
fedha.
“Leo
anataka (Zitto) tuangalie mfumo badala ya majina, nakumbuka katika Bunge la
Tisa, mimi nilikuwa nasema tuangalie mfumo lakini Zitto akasema umefika wakati
wa yeye kutoa dukuduku lake atoe taarifa zake na nyaraka alizonazo ili watu hao
washughulikiwe.”
Werema
anasema kuwa, katika kujaribu kupata taarifa kwa Zitto, mbunge huyo amekuwa
akiwakwepa tangu Februari na kuwa, mwishowe mbunge huyo alikiri kwa kiapo mbele
ya kamati hiyo kuwa hana majina wala akauti za fedha hizo.
Ikumbukwe,
awali, Werema alisema, Zitto angekuwa tu sehemu ya watu wanaosaidia timu hiyo,
lakini kauli yake bungeni juma lililopita, inaonekana kama Zitto ndiye
aliyekwamisha zoezi zima la utafutaji wa fedha hizo.
Werema
hakuzungumza hata kidogo juu ya nini ambacho mpaka sasa tume yake aliyosema
imejaa watalaamu wamefanya, zaidi alitaka aongezewe miezi sita ili akamilishe
kazi hiyo.
Inabidi
Werema aseme ni nini kinamkwamisha kumaliza kazi hiyo ilihali ana kila kitu
kinachotakiwa, fedha pamoja na watu wa kuifanya shughuli hiyo. Pia kwa nini
serikali inasita kusaini sheria hiyo ya kubadilishana taarifa za kifedha kweli
itakuwa njia rahisi za kupata taarifa hiyo.
Kwani licha ya kuwa na rasilimali zote, anang’ang’ania Zitto ataje
majina, kama njia pekee ingekuwa ni mbunge huyo kutaja majina hayo, kwa nini
kamati hiyo iliundwa?
0 comments:
Post a Comment