GOLOSO LA SPORT
NA (YUDATHADEI KWAY)
JE NI KWELI MOYES NI MRITHI WA FERGUSON?
Inaaminika na walio wengi ya
kwamba mtu makini anaelezea maendeleo katika wakati uliopo kwenye nyanja yoyote
ile ni vyema akawa anatoa na historia ya hali ilivyokuwa katika kipindi cha
nyuma. Kwa kuanza hivyo sinabudi ninapotaka kumgusia David Moyes kumzungumzia
Sir Alex Ferguosn pindi akiwa kama meneja wa Manchester United.
Jina halisi la kocha huyu mstaafu
na aliegusa kiaina yake mioyo ya wadau wa soka ni Sir Alexander Chapman
‘’Alex’’ Ferguson. Alijiunga na kikosi cha Man U mnamo November 1986 kama
mrithi wa kocha Sir Matt Busby. Kipindi akipewa timu hii hali ilikuwa mbaya
kisoka klabuni hapo mbali na changamoto hiyo alikuta wachezaji hawana nidhamu
ya kutosha kama vile kuwa na wachezaji walio walevi wa kupindukia akina Norman
Whiteside, Paul McGrath na Brayan Robson hali hii ilimtisha sana kocha huyu ila
alijitahidi vilivyo katika kukabiliana na hali ya nidhamu.
Kipindi akikabidhiwa mikoba timu
ilikua katika nafasi ya 21 ya pili kutoka mwisho, Kocha huyu alijitahidi na
akiwa na wachezaji hawahawa hadi kujikita katika nafasi ya 11 katika msimu wa
1986/1987 hali iliokuwa ya kutia moyo kwa waajiri wa kocha huyu na hata kwa
mashabiki wa timu hii. Katika msimu uliofuata wa 1987/1988 kocha huyu aliongeza
nguvu kwenye kikosi kwa kuwasainisha mkataba wachezaji wanne Steve Bruce, Viv
Anderson, Brian McClair na Jim Leighton. Nguvu hii iliiwezesha timu hii kufikia
nafasi ya pili ya msimamo wa ligi points 9 nyuma ya Liverpool. Msimu uliofata
1988/1989 kocha huyu alimrejesha klabuni hapo Mark Hughes kutokea Barcelona lakini
hali haikuwa nzuri sana kwa klabu hii kwani ilimaliza msimu wa ligi kuu kwa kuwa
katika nafasi ya 11.
Katika msimu wa 1989/1990 kocha
huyu alifanya kufuru kwa kuvunja sefu ya klabu hii kwa kuwasajili Neil Webb, Mike
Phelan, Paul Ince na winga machachari Danny Wallee. Hali haikuwa kama matarajio
yake na wafuasi wake yalivyolenga kwani katika mechi nane za kwanza za ligi kuu
timu ilifungwa mechi 6 na kudroo mbili. Mashabiki na vyombo vya habari kwa
pamoja vilimshambulia vikali na hata wengi wao kudai board ya klabu hio
imuondoshe katika wadhifa wake kama kocha, Lakini board haikuwa na papara kwani
walimuahakikishia kocha huyu msikochi kutofukuzwa kwani waliikubali sababu yake
yakuwa timu ilifungwa kutokana na kwamba wachezaji muhimu walikuwa
wakisumbuliwa na majeraha. Hali hii ilimpatia amani na kujiamini katika kazi
yake na mwisho wa siku alifanikiwa kuchukua kombe la ‘’FA Cup’’ kwa kuifunga
timu ya Crystal Palace bao 1-0 katika mechi ya marudiano baada ya kutoka 3-3
katika mechi ya kwanza. Katika msimu uliofuata wa 1991/1992 klabu ilifanikiwa
kubeba vikombe viwili UEFA supercup na League Cup. Katika msimu wa 1992/1993 Kocha
huyu alimsainisha straika makini kabisa mfaransa akitokea Leeds United kwa
kitita cha Euro million 1.2, huyu ndiye Eric Cantona. Mpachika mabao huyu
aliweza kuuwasha moto katika safu ya ushambuliaji akiwa na mchochea kuni wake Mark
Hughes na mwisho wa msimu klabu hii iliweza kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi
kuu ya Uingereza na kukata kiu cha muda mrefu kabisa, takribani miaka 26 bila
kutwaa kombe hilo.
Katika msimu uliofuata klabu hii
ilimsajili Roy Kean kwa kitita cha Euro Million 3.75, katika msimu huu klabu
iliweza kuchukua vikombe viwili. FA cup kwa kuichapa Chelsea 4-0 katika fainali
na Kutwaa kwa mara nyingine kombe la ligi kuu na kumtoa mfungaji bora Erick
Cantona.
Mafanikio yaliendelea kudhihirika
chini ya kocha huyu na kutia fora katika msimu wa 1998/1999 kwa kuchukua
vikombe vitatu kwa mkupuo, kuanzia klabu bingwa Ulaya(UEFA) ligi kuu Uingereza
na FA Cup.
Tayari kocha huyu aliweza kukonga
nyoyo za wadau wa soka, sio wale tu waliokuwa
kama mashabiki wa Man U lakini hata mashabiki wa klabu nyingine na hata
kudhihirisha ubora na ukomavu wake katika soka. Lilikuwa pigo ambalo si rahisi
sana kufutika kwa miaka ya hivi karibuni katika tasnia ya soka la vilabu, soka
linaloaminika kuwa msingi bora kwa kukua kwa soka katika michuano ya mataifa
mbalimbali kama kombe la dunia na hata makombe ya mabara kwa kocha huyu kuamua
kustaafu na kumpendekeza aliyekuwa kocha wa Everton kwa kipindi hicho David
Moyes kuwa mrithi wa mikoba yake.
Baada ya kuitizama historia fupi
ya Kocha babu Sir Alex akiwa na kikosi cha Man U tujaribu kumgeukia kocha
mrithi aliepewa jina la ‘’Dithering Dave’’ na mashabiki wa Everton. Kocha huyu
aliweza kufanya makubwa akiwa na kikosi cha Everton alicho kabidhiwa mwaka 2002
na hata kufanikiwa kuipeleka timu hio katika michuano ya klabu bingwa katika
mwaka 2005 na hata kufikia hatua ya fainali katika kombe la FA mwaka 2009. Kocha
huyu alidhihirika kuwa kati ya makocha bora kwa vigezo kwa kuwa hakuwa na
wachezaji wa gharama sana katika kikosi chake na bado waliweza kutandaza soka
maridadi kabisa katika ligi kuu ya Uingereza. Timu yake iliweza kuwa ndani ya
kumi bora katika misimu mingi tu ya ligi kuu.
Kocha huyu tokea amekabidhiwa
kikosi cha Man U hajaweza kudhihirisha ubora wake kwani ameishia kupoteza mechi
nyingi katika michuano mbalimbali, ikiwemo kutolewa katika kombe la FA na kufungwa
mechi ya nusu fainali ya mkondo wa kwanza kombe la Capital One. Bado
kocha huyu analegalega katika EPL akitoa matamko ya kuwa timu ni dhaifu. Maswali
yanaibuka, ni vipi anasema timu ni dhaifu alihali Kocha aliepita alitumia wachezaji
hawa hawa kutwaa ubingwa wa EPL? Kama aliona timu ni dhaifu ni kwanini
hakufanya usajili katika majira ya joto? Je ataweza kusajili watu makini katika
dirisha hili dogo? hapa ndipo zinakuja zile sababu za ukomavu na ubora wa kocha
aliyepita. Mengi yanaongelewa na mengi yanatokea ikiwemo kushuka kwa mapato ya
klabu na hata mashabiki kukosa morali ya kuishabikia timu yao kwa kifua mbele kama
ilivyokuwa enzi za Kocha Sir Alex. Man U ni kati ya klabu zinazo sifika kwa
uvumilivu kwa makocha wake, bado ni mapema kwa kocha huyu kufungashiwa virago
tukirejea katika historia ya klabu lakini pia kwa kocha mwenye hekima kisoka ni
muhimu kutumia mbinu mahususi katika kurejesha ubora na umakini wa klabu kama
ilivyokua imetengenezwa na kocha mstaafu Sir Alex Ferguson.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI MSANIFU WA GOLOSO KWA HABARI ZA KIMATAIFA
0768-154424
0 comments:
Post a Comment