GOLOSO LA SOKA
Na Yossima Sitta & yudathadei kway
SOKA
KATIKA UHALISIA WAKE
Swali
likiulizwa, Je ni mchezo gani maarufu zaidi duniani? Bado linabaki kuwa swali
lenye utata kwa maana ya kwamba umaarufu kimchezo unaweza kuwa ;mchezo
unaoangaliwa na wadau walio wengi kwa maana ya kuamasika na mchezo husika au
inaweza kuwa mchezo uliochezwa kwa muda mrefu zaidi duniani au unaweza kuwa
mchezo wenye kuingiza mapato zaidi duniani. Katika kulitazama hili la mchezo
wenye hamasa zaidi duniani kwa kuangaliwa na kufuatiliwa na walio wengi, tafiti
za kina zimefanyika kimataifa na imebainika kuwa watu wapatao 3.3-3.5 bilioni kutoka katika
mabara mbalimbali (Ulaya,Africa, Asia ,Americas ,n.k) ni wakereketwa wa mchezo
wa soka, mpira wa miguu. Takwimu hizi ni kati ya jumla ya watu wanao kadiriwa
kufikia billion 7.137 Dunia nzima kulingana na taarifa iliotolewa na United
States Census Bureau (USCB ) hapo 12,March,2012. Tukiingia ndani zaidi kitafiti inaonyesha mchezo huu unakadiriwa kuchezwa na wachezaji
million 250 katika nchi zipatazo 200 na kudhihirisha kuwa mchezo maarufu zaidi
katika sayari hii. Michezo inayofuata kwa umashuhuri ni pamoja na Cricket wenye
wakereketwa wapatao 2-3 billion. Field Hockey wenye mashabiki wanaofikia 2-2.2
billion na mchezo huu ni maarufu zaidi katika nchi za Asia, Ulaya, Australia, n.k
ukifuatiwa na Tennis mchezo wenye mashabiki wapatao billion 1 zaidi katika nchi
za Ulaya, Americas na Asia.
Katika
kujikita kisoka zaidi kuna sababu nyingi zinazo jaribu kuthibitisha ni kitu gani
kinachofanya mpaka watu kuvutiwa na mchezo huu zaidi na hata wengi wao kudiriki
kukiri ya kuwa hawana sababu maalumu isipokuwa wamejikuta wakiupenda tu. Hili
liko wazi hata kwa wale walio na uzoefu kama sio professionals katika uliwengu
wa mapenzi mtu akimpenda mwenzi wake basi kama sio kwa sababu za tamaa tamaa
tu, Huwa ni ngumu kuwa na sababu ya moja
kwa moja iliomfanya au inayomfanya
kumpenda mwenzi wake zaidi inabaki kuwa ni uhalisia usio elezeka kirahisi. Hii
ndio sababu nzito zaidi kwa walio wengi katika upenzi wa mchezo huu
tajwa.Tumepata kusikia matukio mengi yanayoendana na upenzi katika tasnia hii
ya soka, Kama vile watu kujiua kisa timu zao kufungwa, mashabiki kuuawa kisa tu
mashabiki kuwa wengi kuliko ukubwa wa uwanja. Watu kucheza kamari na hata
kujivunia mengi yaliyo ya thamani na hata wengine kusadikika kuwaweka wake zao
rehani kisa tu ni upenzi uliokithiri juu ya mchezo huu mashuhuri zaidi. Lakini
kupitia mchezo huu vijana wengi wanajipatia ajira tena zenye ujira wenye
kuridhisha kabisa na zaidi ni nchi nyingi kufaidika kiuchumi kupita mchezo huu
kama vile kwanjia ya michuano mbalimbali inayowaleta pamoja katika eneo moja
umati wa watu kutoka maeneo mbalimbali nje na eneo husika.
Mengi
yanafanyika katika harakati za kuufanya mchezo huu kuwa bora kila kukicha, baadhi
ya mambo yaliofanyika kupitia mashirikisho ya soka duniani ni pamoja na
kuanzisha soka la wanawake na hata kufikia hatua ya kombe la dunia la wanawake
na hivyo kutanua wigo, nikimaanisha hapo kabla mchezo huu ulikuwa ukiwahusisha
wanaume tu lakini sasa hata wanawake wanajikakamua kwenye pitch. Bila kusahau
Shirikisho la mpira wa miguu ulaya(UEFA) kuboresha maamuzi uwanjani kwa kuweka
vibendera wanne mmoja kwa kila upande wa pitch. Bila kusahau shirikisho la soka
la Uingereza(FA) kuanzisha teknolojia ya goli katika kutambua goli kama ni
halali au la.
Jitihada
pia zinafanyika katika ngazi za vilabu ikiaminika ya kuwa ubora wa mpira katika
timu za taifa unachangiwa zaidi na nguvu kubwa katika vilabu. Katika soka imani
ziko nyingi lakini zaidi ninalotaka kuligusia katika kipengele hiki ni wimbi la
kuwaamini walioishakuwa wachezaji kuwa mameneja katika timu mbalimbali. Jambo
hili linatafsiriwa na wanamichezo kama jambo lenye tija zaidi katika kuleta
ladha kamili kisoka kwani meneja aliyeisha kuwa mchezaji ni wazi ya kwamba
anatambua ni nini kifanyike uwanjani na nani na katika muda gani na mwisho wa
siku kutarajia matokeo mazuri.
Haya
yameshuhudiwa na watabe waliowika enzi
hizo na mwisho wa siku kukabidhiwa mikoba ya ukocha. Baadhi wakiwemo Frank Rijkad aliekuwa
akiifundisha Barcelona na hata kufanya makubwa akiwa na masupa staa kama
Ronaldinho Gaucho na Samwel Eto’o, Akaja Pep Gaudiola
aliyekuwa kiungo mkabaji kipindi cha enzi zake na baadae kuwa kocha
katika timu ya Barcelona B baadae Barcelona ya wakubwa kuanzia mwaka 2008-2012.
Ambapo katika kipindi hicho alifanya maajabu katika tasnia ya soka la vilabu na
baadae katika msimu huu kupewa mikoba ya kuinoa klabu mashuhuri duniani inayosifika kwa mpira wenye hekima nikimaanisha ina wachezaji
wenye sifa za kucheza mpira wenye kasi, nguvu na umakini katika kupiga pasi na
kufunga hawa ni Bayern munich mabingwa watetezi wa kombe la UEFA. Wako makocha
wengi walio aminiwa na kupewa majukumu hayo na walishafanya makubwa kwenye
pitch wakiwemo Meki Mexime ‘’kaptani’’ Seleman Matola, Dunga, Diego Maradona na
wengine wengi. Katika wiki hii tumeshuhudia pia klabu ya Ac Milan ikifanya maamuzi
mazito kwa kumfukuza aliye kuwa kocha wake Massimiliano Allegri na kumkabidhi
mikoba kiungo wa timu hiyo ambaye alikaa kwa kipindi cha miaka kumi mdachi
Clarence Seedorf. Yamesemwa mengi na walio wengi na wengi wao wakitegemea makubwa katika klabu hio
iliyokuwa na mwanzo mbaya katika ligi kuu ya Italia maarufu kwa Serie A.
Hizi
zooooote ni mbwembwe za soka mchezo unaosadikika kuanza kuchezwa katika nchi ya
China (karne ya 2 na 3 Kabla ya Kristu) na kusemekana ya kuwa waingereza ndio
walio boresha mchezo huu kama tunavyo uona hivi leo. Soka ndiyo habari ya mjini
na vijijini, mashuleni na vyuoni, watoto, vijana, rika la kati na hata wazee Kuongelea
soka kila siku.
waandishi wa makala hii
Yossima Sitta (mhariri & afisa habari wa goloso)
Yudathadei Kway (msanifu wa habari za kimataifa wa goloso)
0 comments:
Post a Comment