Pages

Friday, 10 January 2014

SUNZU NA SINKALA WA TP MAZEMBE WAMFUUTA KOCHA WAO UFARANSA




Licha ya mmiliki wake, Moise Chapwe Katumbi kusisitiza kuwa TP Mazembe itarudi kwa nguvu Zaidi na kucheza fainali za klabu bingwa duniani mwaka huu, bado ni dhahiri kuwa vigogo hao wakongo wana kazi ya kujenga upya kikosi chao.
Inawezekana TP Mazembe wakaja na nguvu Zaidi kama mmiliki wake anavyodai hasa ukizingatia kuwa fungu la kufanya usajili wa nguvu kuziba mapengo si shida. Pesa za kufanya usajili wa nguvu wanazo, lakini je wataweza kujenga timu yenye umoja kwa haraka haraka kiasi cha kunyakua ubingwa wa Afrika na kukata tiketi ya kufuzu klabu bibgwa duniani ndani ya mwaka mmoja?
Kinara wa ulinzi Stophila Sunzu pamoja na Mzambia mwenzake, Nathan Sinkala wamekwisha ondoka. Sunzu na Sinkala wamefanikiwa kujiunga na klabu ya Sochaux ya Ufaransa. Wanaungana na kocha wao kipenzi, mfaransa Herve Renard.
Kuondoka kwa Sunzu na Sinkala kunaacha pengo kubwa. Mwaka jana, safu ya ulinzi ya Mazembe iliyumba sana kwa kumkosa Stophila Sunzu. Ikumbukwe Mazembe walikuwa wanasifika kwa kutoruhusu mabao, iwe nyumbani au ugeni. Bila ya Sunzu, ukuta wa Mazembe ulijikuta ukiruhusu mabao matatu dhidi ya Orlando Pirates katika mechi ya raundi ya pili ya ligi ya mabingwa Afrika. Safari yao ya kwenye ligi ya mabingwa Afrika ikawa imeishia hapo baada ya kuambulia ushindi mwembamba wa 1-0 kwenye mechi ya marudiano.
Licha ya mabao ya Mbwana Samatta kuwasukuma hadi fainali ya kombe la shirikisho, bado ukuta wao ulionekana kuwaangusha. Tisa kumi, sakata la uhamisho wa nahodha wao tegemeo, Tressor Mputu bado halijafika mwisho. Unapotaja mpira wa Kongo, ni sharti utaje TP Mazembe, na unapoitaja Mazembe ni sharti jina la Mputu liongelewe. Mputu ni kama taasisi, ni kiongozi, ni mhamasishaji na silaha ya ushindi katrika klabu ya Mazembe.
Naijaribu kutafuta picha ya TP Mazembe bila ya Sunzu, Sinkala na Mputu. Napata shida kuona Katumbi akiwaruhusu nyota wake Zaidi waondoke huku akiwa na ndoto za kuwa klabu ya kwanza Afrika kutwaa ubingwa wa dunia.
Bila shaka uhamisho wa Sunzu na Sinkala utakuwa umewaongezea kiu ya kucheza Ulaya Samatta na Ulimwengu. Kuondoka kwa Sunzu na Sinkala kunaweza kuwa kumewafungulia milango au kumewafungia dirisha.
Iwapo Sunzu na Sinkala watang’aa na kuiokoa Sochaux kutoka kwenye dimbwi la kushuka daraja basi mawakala wan je wanaweza kuongeza kasi ya kuimulika TP Mazembe ili kuangalia ‘madini’ mengine. Hii inaweza kuwa bahati ya kina Samatta na Ulimwengu.
SOURCE: shaffih dauda blog

0 comments:

Post a Comment